BARCELONA ndiyo mabingwa wapya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, hiyo siyo
habari mpya kwa sasa lakini habari ni kuwa kwa nini Barcelona?
Wapo ambao wamekuwa wakimtazama Lionel Messi kuwa ndiye nguzo muhimu
kwa timu hiyo kutwaa mataji matatu msimu huu, hilo ni kweli lakini hali halisi
ni kuwa Barcelona imeshinda taji hilo kwa kuwa kila mtu kwenye timu kafanya
kazi yake vizuri.
Messi amekuwa akionekana zaidi kwa kuwa uwezo wake ni wa kipekee na
amekuwa akionyesha makubwa zaidi hata ya wenzake lakini baada ya kuanza msimu
kwa kuyumba, hatimaye Barcelona ilianza kuelewana na kufanya kila mtu kucheza
kwa kiwango cha juu.
Ushirikiano wa Messi, Neymar na Luis Suarez unastahili pongezi za
kipekee kwa kuwa hawakuwa wachoyo, ndiyo maana hata juzi wawili kati yao
walifunga huku mmoja akitengeneza mabao.
Fainali vs Juventus
Katika fainali ya juzi dhidi ya Juventus ambapo Barcelona ilishinda
3-1, usiku kipa chipukizi Marc-André ter Stegen, 23, hakuwa na kazi kubwa
lakini alionyesha kujiamini, anaonyesha dalili za kuwa kipa bora miaka ijayo,
hasa kama ataendelea kubaki klabuni hapo.
Mabeki wote walikuwa kwenye ubora wao, Dani Alves kama kawaida
alisaidia mashambulizi kwa kupanda, japokuwa mara kadhaa alijisahau na Juventus
kupata nafasi ya kupiga krosi kadhaa kutoka upande wake.
Gerard Pique ndiye beki aliyecheza vizuri kuliko wote, alipanda
kusaidia mashambulizi, aliokoa vizuri, alicheza mipira ya juu na aliwapanga
wenzake vizuri. Javier Mascherano alianza kwa kupaniki lakini baadaye alitulia
na kuonyesha ubora wake.
Jordi Alba kama ilivyo kwa Alves alipanda mara nyingi na kuchangia bao
la kwanza, hakuwa na kazi nzito ya kukaba.
Katika safu ya kiungo, ushirikiano wa Sergio Busquets na Ivan Rakitić ulikuwa na maana, wao ndiyo waliozima mashambulizi ya Juventus kutokea katikati.
Mkongwe Andrés Iniesta ndiye aliyekuwa injini ya Barcelona, kwa kuwa
vijana wake wawili nyuma walifanya kazi nzuri, hiyo ilimrahisishia kuuchezea
mpira, kuiendesha timu, kutoa pasi zenye macho na kuituliza Barcelona hasa
mwanzoni mwa kipindi cha pili ambapo walionekana kupoteana kiasi.
Messi inawezekana hakuonyesha yale makeke yake ya kuukokota mpira na
kuwapangua wapinzani lakini yeye na Iniesta ndiyo waliokuwa mafundi mitambo.
Messi alianza kutengeneza bao la kwanza kwa pasi yenye macho, kisha
akatengeneza la pili ambalo lilitokana na ule uwezo wake binafsi ambao
unajulikana.
Suarez licha ya kuwa staika wa kati lakini alifanya kazi nzuri ya
kuwasumbua mabeki wa Juventus, kuna muda alirejea katikati ya uwanja ili
kumsumbua Andrea Pirlo pindi Juventus walipokuwa wakimiliki mpira.
Kocha wa Barcelona, Luis Enrique alipanga kikosi kizuri na mbinu zake
zilifanikiwa. Mabadiliko aliyoyafanya yalikuwa na maana kubwa na faida, Jérémy
Mathieu aliingia kuzuia, Juventus wakapanda kujua wapinzani wao wamezidiwa,
wakajikuta wanapigwa la tatu kwa shambulizi la kushtukiza.
Moja ya vituko baada ya mechi kuisha ni mlinzi wa Barcelona Gerald Pique akikata nyavu kwa kutumia mkasi |
Pique akiwa kajifunika nyavu |
Messi akiwa anashangilia kwa kulibeba kombe la Ulaya |
Neymar akilibusu kombe |
No comments:
Post a Comment