BENJAMINKAMINYOGE.BLOGSPOT.COM

Wednesday, October 29, 2014

RAIS WA ZAMBIA MICHAEL SATA AFARIKI JIJINI LONDON

  Kifo chake kimetokea siku chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo. Mwanasiasa huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya kuongoza chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party Democracy, kikiwa madarakani kwa miaka ishirini.
 Michael Chilufya Sata alizaliwa mwaka 1937 katika mji wa Mpika, eneo ambalo lilikuwa wakati huo ni Northern Rhodesia. Muumini wa dini ya Kikristo ya madhehebu ya Katoliki, alifanya kazi kama afisa polisi, mfanyakazi wa reli na mwanachama wa chama cha wafanyakazi wakati wa utawala wa kikoloni. Baada ya Zambia kupata uhuru wake, pia aliishi kipindi fulani mjini London, akiwa mfanyakazi wa reli, na kurejea Zambia, akiwa na kampuni ya teksi.
 Akiwa mwenye sauti ya mkwaruzo yakiwa ni matokeo ya kuvuta sigara kwa muda mrefu, Bwana Sata aliibuka katika siasa na kupata umaarufu katika miaka ya 1980. Haraka akapata sifa ya kuwa gavana mwenye kuchapa kazi kwa bidii, wakati akiongoza jimbo la Lusaka na mtu wa utekelezaji kwa vitendo.
 Lakini pia alijulikana kama mtu wa kutoa amri, mtu asiyeendekeza urafiki na mkali na wapinzani wake walisema jina alilopewa la bandia la "King Cobra" alikuwa anastahili kuitwa hivyo. Kwa mara ya kwanza alionekana kama mtu ambaye angetekeleza ahadi za kupambana na rushwa na kupata ufumbuzi wa tatizo la ajira na kuleta ustawi wa jamii. Lakini kipindi chake madarakani kiligubikwa na kuuzima upinzani wa kisiasa na kudorora kwa uchumi. Bwana Sata ni rais wa pili wa Zambia kufariki dunia akiwa madarakani baada ya Levy Mwanawasa.
Rais Michael Sata Enzi za uhai wake

No comments:

Post a Comment