BENJAMINKAMINYOGE.BLOGSPOT.COM

Monday, June 08, 2015

BARCELONA MABINGWA ULAYA 2014/15


BARCELONA ndiyo mabingwa wapya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, hiyo siyo habari mpya kwa sasa lakini habari ni kuwa kwa nini Barcelona?


Wapo ambao wamekuwa wakimtazama Lionel Messi kuwa ndiye nguzo muhimu kwa timu hiyo kutwaa mataji matatu msimu huu, hilo ni kweli lakini hali halisi ni kuwa Barcelona imeshinda taji hilo kwa kuwa kila mtu kwenye timu kafanya kazi yake vizuri.

Messi amekuwa akionekana zaidi kwa kuwa uwezo wake ni wa kipekee na amekuwa akionyesha makubwa zaidi hata ya wenzake lakini baada ya kuanza msimu kwa kuyumba, hatimaye Barcelona ilianza kuelewana na kufanya kila mtu kucheza kwa kiwango cha juu.


Ushirikiano wa Messi, Neymar na Luis Suarez unastahili pongezi za kipekee kwa kuwa hawakuwa wachoyo, ndiyo maana hata juzi wawili kati yao walifunga huku mmoja akitengeneza mabao.

Fainali vs Juventus
Katika fainali ya juzi dhidi ya Juventus ambapo Barcelona ilishinda 3-1, usiku kipa chipukizi Marc-André ter Stegen, 23, hakuwa na kazi kubwa lakini alionyesha kujiamini, anaonyesha dalili za kuwa kipa bora miaka ijayo, hasa kama ataendelea kubaki klabuni hapo.

Mabeki wote walikuwa kwenye ubora wao, Dani Alves kama kawaida alisaidia mashambulizi kwa kupanda, japokuwa mara kadhaa alijisahau na Juventus kupata nafasi ya kupiga krosi kadhaa kutoka upande wake.

Gerard Pique ndiye beki aliyecheza vizuri kuliko wote, alipanda kusaidia mashambulizi, aliokoa vizuri, alicheza mipira ya juu na aliwapanga wenzake vizuri. Javier Mascherano alianza kwa kupaniki lakini baadaye alitulia na kuonyesha ubora wake.

Jordi Alba kama ilivyo kwa Alves alipanda mara nyingi na kuchangia bao la kwanza, hakuwa na kazi nzito ya kukaba.

Katika safu ya kiungo, ushirikiano wa Sergio Busquets na Ivan Rakitić ulikuwa na maana, wao ndiyo waliozima mashambulizi ya Juventus kutokea katikati.

Mkongwe Andrés Iniesta ndiye aliyekuwa injini ya Barcelona, kwa kuwa vijana wake wawili nyuma walifanya kazi nzuri, hiyo ilimrahisishia kuuchezea mpira, kuiendesha timu, kutoa pasi zenye macho na kuituliza Barcelona hasa mwanzoni mwa kipindi cha pili ambapo walionekana kupoteana kiasi.

Messi inawezekana hakuonyesha yale makeke yake ya kuukokota mpira na kuwapangua wapinzani lakini yeye na Iniesta ndiyo waliokuwa mafundi mitambo.

Messi alianza kutengeneza bao la kwanza kwa pasi yenye macho, kisha akatengeneza la pili ambalo lilitokana na ule uwezo wake binafsi ambao unajulikana.

Suarez licha ya kuwa staika wa kati lakini alifanya kazi nzuri ya kuwasumbua mabeki wa Juventus, kuna muda alirejea katikati ya uwanja ili kumsumbua Andrea Pirlo pindi Juventus walipokuwa wakimiliki mpira.

Kocha wa Barcelona, Luis Enrique alipanga kikosi kizuri na mbinu zake zilifanikiwa. Mabadiliko aliyoyafanya yalikuwa na maana kubwa na faida, Jérémy Mathieu aliingia kuzuia, Juventus wakapanda kujua wapinzani wao wamezidiwa, wakajikuta wanapigwa la tatu kwa shambulizi la kushtukiza.

Xavi Hernandez aliingia kuituliza timu na akafanikiwa kwa hilo, Pedro ni mjanjamjanja na ndiye aliyesaidia bao la tatu.
Moja ya vituko baada ya mechi kuisha ni mlinzi wa Barcelona Gerald Pique akikata nyavu kwa kutumia mkasi

Pique akiwa kajifunika nyavu
Messi akiwa anashangilia kwa kulibeba kombe la Ulaya
Neymar akilibusu kombe

No comments:

Post a Comment