BENJAMINKAMINYOGE.BLOGSPOT.COM

Tuesday, October 07, 2014

RAIS UHURU KENYATTA KIZIMBANI THE HAGUE

  Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameondoka nchini humo leo kuelekea The Hague ili kuhudhuria kikao juu ya kesi inayomkabili katika mahakama ya kimataifa –ICC
  Jumatatu Bw. Kenyatta alitoa hotuba isiyo ya kawaida kwa wabunge na maseneta iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari na kwenye mtandao wa internet.   Katika hotuba hiyo Bw. Kenyatta alimkabidhi madaraka ya muda naibu rais William Ruto ili aweze kwenda Uholanzi bila kuacha pengo la madaraka. Alisema anakwenda kwenye mahakama hiyo kama mwananchi wa 'kawaida' na kusisitiza kuwa kamwe hana hatia. Yeye pamoja na naibu rais Ruto, wanashtakiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka wa 2007, ambapo maelfu ya wakenya waliuawa na wengine wengi kulazimika kutoroka manyumbani mwao. Katika uchaguzi huo, rais wa zamani Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walikuwa wanagombania urais. Bwana Kenyatta hata hivyo na mgombea mwenza William Ruto walichaguliwa na Wakenya kuongoza taifa hilo na kuapishwa mwezi Aprili mwaka 2013. Wote wawili wamekanusha kuhusika na ghasia hizo na wameshirikiana na mahakama hiyo ya ICC. Ni mara ya kwanza kwa rais anayehudumu kuwa katika mahakama hiyo ya kimataifa. Kesi ya Bw. Kenyatta itasikilizwa Jumatano.

No comments:

Post a Comment