BENJAMINKAMINYOGE.BLOGSPOT.COM

Monday, September 22, 2014

STAND UNITED WAMILIKI WAKE NI WAPIGA DEBE NA MAKONDA KIHALALI,TUNAJIFUNZA NINI?SISI WENYE MAKAMPUNI.


Hiki ndio kikosi cha Stand United
 UKITUA katika Mkoa wa Shinyanga, hususan maeneo ya stendi ya zamani ya mabasi ya mikoani na wilayani, utakutana na shamrashamra za makonda, madereva na wapiga debe ambao wanaendelea na shughuli zao za kujipatia riziki. Lakini hao makonda, wapiga debe, mawakala na madereva, ndiyo chachu na mafanikio ya Stand United, kwani wao ndiyo waanzilishi na wamechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya timu hiyo ifike hapo ilipo tangu ilipoanzishwa mwaka 2012.  Stand inaongozwa na viongozi wenye uchungu na mpira na uchu wa mafanikio katika soka, ndiyo maana wamefanikiwa kwa kiasi fulani. Wanaendesha timu huku wakiendelea na majukumu yao ya kila siku na kazi zao, ingawa wanahakikisha kila kitu kinakuwa kinaenda sawa kabisa bila tatizo katika mabasi wengine maduka yanayozunguka eneo hilo la stendi. Unapofika Stand, unakutana na makamu mwenyekiti wa timu hiyo, Masumbuko Charles ambaye ni mmoja wa mawakala wa basi la Loquman ambalo linafanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka wilaya za Meatu na Bariadi hadi mkoani Dodoma. Licha ya Masumbuko kuwa na majukumu mengi, timu inapofanya mazoezi huwezi kumkosa. “Uwepo wangu katika timu hii ni furaha kwa sababu ilikuwa ndoto yetu hapa tangu muda na imefanikiwa kutimia kwa kiasi mpaka hapa tulipofika, tutapigana kwa sababu mwanzo tulikuwa tunasumbuliwa na ukata lakini tumetimiza ndoto kwa kiasi,” anaeleza Masumbuko. Rashid Daghesh ambaye ni kocha wa kwanza wa Stand kwa sasa ni mjumbe wa kamati kuu ya timu hiyo huku aliyekuwa msaidizi wake Aman Vincent akiwa ndiye mwenyekiti wa timu kwa sasa. Rashid, pamoja na majukumu ya timu aliyonayo, pia ni wakala wa mabasi ya Ruska ambayo yanafanya shughuli zake mkoani humohumo. “Kitu ambacho naweza kujivunia Stand United ni pamoja na kuifanya timu kuwa hapa ilipofika sasa, kwa sababu zamani wakati nacheza timu yangu haikuwa na bahati ya kufika ligi kuu, sasa imepiga hatua, ni jambo la kheri,” anasema Rashid.  Mohamed Ally Hemed ‘Dulla’ yeye ni mmoja wa wadau walioanza kuisapoti timu tangu inaanza, akiwa ni mfanyakazi wa hapo na anamiliki basi la Bedui Ruska ambalo ameamua kuweka jina kubwa la timu katika basi hilo. “Naipenda sana timu hii popote iendapo huwa naisapoti kwa kiasi kikubwa tangu tumeanza kuichangia Sh 500 kipindi hicho,” anaeleza. Araf Nassor akiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Stand United naye ni wakala wa mabasi ya Ruska lakini akiwa pia ni mmoja wa waasisi wa timu. “Timu imepiga hatua kwa kiasi kikubwa lakini napenda kuwaambia Watanzania kuwa, Stand United si timu ya wahuni, wala wafanya fujo, sisi ni watu wa malengo, ndiyo maana tumefika hapa, japo ukata kwa sana lakini tunapigana kuendesha timu,” anasema Nassor. Je, mashabiki wanaisapoti vipi timu? “Timu ilipokuwa ikienda mikoani, kipindi hicho walikuwa wanagharamiwa na timu kwa kupitisha mabakuli na kuchangisha na hawa mashabiki wetu wapo katika makundi mawili, Full Shangwe ambao muda wote wanaishangilia timu pamoja na Babu Kubwa, wote hawa ni mashabiki wa timu yetu. “Pia kwa sasa baada ya kupanda, mtashuhudia Bendi ya Stand ikitoa burudani katika michezo yake tofauti wakati ligi kuu itakapokuwa ikiendelea,” anafafanua Nassor. Hao ni baadhi ya wadau na viongozi wa Stand United ambao wamekuwa na timu tangu inaanza mpaka hapo ilipofikia, ingawa haikuwa kazi rahisi kufika hapo walipofika.

No comments:

Post a Comment